Viazi Lishe na Fursa Zilizo Ndani Yake.

Viazi Lishe na Fursa Zilizo Ndani Yake.

Viazi lishe ni aina ya viazi vitamu vyenye mwonekano wa rangi ya njano kwa ndani vikimenywa. Viazi lishe ni biashara mpya katika kilimo biashara ambacho hakijamulikwa vyema na wakulima wetu.

Hii ni fursa muhimu na ya kipekee kwa wakulima wanaolenga utajiri kutokana na kilimo. Kwa kifupi huku kuna pesa kuliko kawaida. Ni muhimu tukaichangamkia fursa hii. Kilimo cha viazi lishe ni kama ilivyo kwa viazi vingine vitamu ni rahisi sana ukilinganisha na aina nyingine ya kilimo.

Viazi lishe hutumia muda wa miezi mitatu toka kupandwa hadi kuvunwa. Na kama vikilimwa kwa ajili ya mbegu, vyazi hivyo hutumia miezi miwili tu na vinakuwa tayari kuvunwa na kupelekwa shambani.

Viazi lishe vina beta karotini ambayo ni chanzo muhimu cha vitamini A. Viazi lishe vinatengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo Chipsi, Kripsi pamoja na Unga ambao hutumika kutengenezea bidhaa mbalimbali kama vile Mikate, Keki, Maandazi, chapati, Biskuti na vitafunwa vinginevyo. Kwa kifupi, kwa kutumia viazi lishe, tunaweza kutengeza bedhaa zote ambazo unga wa ngano unatengeneza. Majani ya viazi lishe hutumika kama mboga.

Ekari moja huitaji mbegu elfu 12 na kila mbegu moja tunaiuza kwa tsh 60/= kwa mteja anayechukua mbegu kuanzia elfu 12 na kuendelea lakini chini ya hapo mbegu moja inauzwa kwa tsh 100/=. Tunatoa huduma ya kukusafirishia hadi ulipo kwa kukupostia mzigo kwenye gari na huduma yetu ni bora sana .

Katika ekari moja una uwezo wa kuvuna tani 19 hadi 24 kutegemeana na matunzo yako. Kwa kawaida mbegu moja ya viazi lishe iliyopandwa inatoa kilo 2 za viazi. Kadiri unavyoweka matuta makubwa ndivyo unatakavyovuna viazi vikubwa zaidi. Upandaji wa viazi lishe kati ya shina moja na jingine ni futi moja moja na kati ya tuta moja na tuta jingine pia ni futi moja.

Viazi lishe ni vitamu sana. Vina unga wa kutosha na mwonekano wake huwavutia wateja wengi sokoni ukilininganisha na viazi vitamu vya kawaidi. Lakini vilevile viazi hivi vimepewa chapuo kubwa na wenzetu wataalam wa lishe kwa ajili kuboresha afya ya watoto, akina mama wajawazito pamoja na wazee.

Kilo moja ya viazi lishe inakwenda kwa tsh 1000/= sokoni. Na shina moja linatoa wastani wa kilo mbili na ekari moja ina mashina 12,000. Kwa haraka haraka ekari moja ikiwa utafuata na kuzingatia masharti yote muhimu utaweza kuvuna tani hadi 24. Sasa wewe rudisha nyuma hiyo hesabu, fanya utavuna tani 20 tu ambayo ni sawa na kilogramu 20,000. Je wajua kwa hiyo ekari moja utaweza kutengeneza tsh ngapi? Hapa utachukua 1000/= X 20,000KGS itakuwa sawasawa na tsh. 20 milioni. Hebu niambie kuna biashara gani unaweza kufanya kwa miezi michache tu ukaibuka na kiwango hicho cha pesa. Fursa ni nyingi mtaani tuzichangamkieni.

Viazi Lishe na Fursa Zilizo Ndani Yake.

Hapo hatujaongealea biashara ya mbegu za viazi hivyo. Navyo ni hela pia. Ukiamua kuzalisha mbegu za viazi lishe kama nilivyosema hapo awali vyenyewe huchukua miezi miwili tu hadi kuvunwa. Katika ekari moja inatoa mbegu laki moja 1,046,000 na kila mbegu kwa bei inauzwa kwa tsh 30/= na sokoni kwa wale wateja wakubwa kabisa wanaochukua kuanzia mbegu 360,000 zinauzwa kwa tsh 50/=. Sasa ukichukua mbegu 1,046,000 x 30/= mkulima ataweza kupata jumla ya tsh 31,380,000/= . Je kuna biashara yeyote unayoweza kufananisha na kilimo hiki cha uzalishaji wa mbegu na viazi vyake?

Ni muhimu kukumbuka viazi ni miongoni mwa mazao yanayostahimili sana ukame hivyo vinamuhakikishia mkulima chakula cha uhakika. Vilevile kilimo hiki cha viazi lishe, hakina usumbufu kama ilivyo kwa aina nyingine ya kilimo. Ukipitisha trakta likavuruga ardhi, ukapanda mbegu kitakachofuata ni palizi tu. Kwa baadhi ya maeneo huhitaji mbolea lakini kuna baadhi ya maeneo mengine kama vile Morogoro hayahitaji hata mbolea, ukivichomeka tu basi utasubiri palizi kisha kuvuna.

Viazi lishe hustawi katika maeneo mengi ya nchi yetu lakini hustawi zaidi katika maeneo ya joto kwa mfano maeneo yote ya mikoa ya Pwani na Morogoro, maeneo yote ya Kanda ya ziwa na mikoa ya magharibi kama vile Tabora na Kigoma, Mikoa ya Kanda ya kati Singida na Dodoma pamoja na mikoa ya nyanda za juu kusini hasa Ruvuma, Rukwa na Katavi. Kwahiyo wakulima waliyo kwenye maeneo hayo wana fursa zaidi ya kuendesha kilimo hiki cha viazi lishe pamoja na mbegu zake.

Source Link

identicon

About Jamii Forums

JamiiForums is a Tanzania-based social networking website in East Africa founded by Maxence Melo and Mike Mushi in 2006. The online network is notable as the most popular social media website in Tanzania

View all posts by Jamii Forums →