KATI ya Julai hadi Septemba mwaka huu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya jumla ya trilioni 3.84 likiwa ni ongezeko la asilimia 5.32 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi hicho mwaka jana.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA Richard Kayombo amesema, mwaka jana katika miezi hiyo ilikusanya shilingi trilioni 3.65.
Amesema, kwa Julai pekee TRA ilikusanya trilioni 1.2/-, Agosti trilioni 1.27/- na Septemba zilikusanywa trilioni 1.36/-.
“Tunawashukuru wote wanaoendelea kulipa kodi zao kwa hiyari na kwa wakati,” amesema Kayombo.
Kwa mujibu wa Kayombo, lengo la TRA ni kukusanya trilioni 18/- za mapato kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Ameonya wafanyabiashara hususani wa Kariakoo, Dar es Salaam wanaoghushi risiti za kielektroniki EFD na kusema watachukuliwa hatua za kisheria.